Wateja milioni 2.5 wa Simu za
rununu leo wamejipata mashakani baada ya Tume ya Mawasiliano nchini
Kenya kuzima simu ghushi.
Zoezi hilo la kuzima simu lilianza kutekelezwa
usiku wa manane na linalenga kukabiliana na uingizaji wa simu bandia,
suala linalohujumu juhudi za kuimarisha usalama.
Hatua ya kuzima simu ghushi na
ambayo imethibitishwa na kampuni nne za huduma za simu nchini humo,
inafuatia agizo la tume ya wasiliano nchini humo ambayo inataka
kukabiliana na biashara haramu, wizi wa haki miliki na tisho la usalama.
Afisaa mkuu mtendaji wa tume hiyo, Francis
Wangusi, alielezea kuwa hatua ya kuzima simu hizo, ambayo ilikuwa
imeakhirishwa mara tatu iliweza kutekelezwa usiku wa kuamkia leo.
Tume hiyo haijashirikiana na kampuni za huduma za simu kuzima simu ghushi tu bali pia simu ambazo wateja wake hawajasajiliwa.
Hatua hii imesababisha hasare kubwa kwa kampuni za simu.
Hata hivyo tume ya CCK, imetenga bajeti ya pesa
itakazotumia kugharamia hasara ya kampuni za simu ingawa wateja wa simu
hizo hawatapata fidia yoyote.
Kampuni ya Safaricom, ambayo ina wateja wengi
zaidi ya kampuni zote za huduma za simu za rununu nchini Kenya,
imezima simughushi, 670,000 katika masaa 15 pekee.
Kampuni ya Airtel Kenya nayo imezima simu
100,000 huku yuMobile ikizima takriban simu 45,000. Kampuni ya Telkom
Orange imezima takriban simu 20,000.
Nani wa kulaumiwa kwa kuingiza nchini simu bandia?